BODABODA WANAVYOITIA HASARA HOSPITALI YA BUGANDO
![]() |
| Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza. |
HOSPITALI ya rufaa ya
Bugando iliyopo jijini Mwanza imekuwa ikipata hasara ya takribani Sh. milioni
tano mpaka milioni 12 kila wiki ikiwa ni misamaha ya gharama za matibabu ya
majeruhi wa ajali za barabarani hususani bodaboda.
Katika mahojiano maalumu
na mwandishi, Afisa Ustawi wa Jamii hospitali ya Bugando, Daudi Makumucha,
alisema, “Gharama kubwa za matibabu zinawatesa majeruhi wengi wanofikishwa
hospitalini.
“Wapo wanaolazimika
kuuza mali zao ili aweza kumudu gharama za matibabu.”
Alisema hali hiyo
inailazimu hospitali hiyo kutoa msamaha wa matibabu kila wiki kwa wagonjwa
ambao hawana uwezo wala ndugu wa kumudu kulipa gharama hizo.
“Leo pekee (Julai 13,
2017) tumejadili mafaili ya wagonjwa kumi na kupitisha msamaha wa madeni kiasi
kinachofikia shilingi milioni tano,….kuna mgonjwa kutoka wodi ya mifupa,
alipata ajali na alikuwa anadaiwa takribani Sh. 2,474,800/-” alisema.
Kwa mujibu wa Makumucha,
majeruhi hao mara nyingi hupata majeraha makubwa na kuwachukua muda mrefu kukaa
hospitali hususan katika kitengo cha uangalizi maalum (ICU).
Mara zingine majeruhi
hufikishwa bila kujitambua, lakini hospitali humtibia mpaka akizinduka ndipo
ndugu zake hutafutwa.
Anaeleza kuwa wapo
wagonjwa ambao hutoroka ili kukwepa gharama za matibabu. Hivyo hospitali kwa
jumla hupoteza Sh. milioni tano mpaka 12, ambapo kwa mwezi inapoteza kati ya
Sh. milioni 20 mpaka 48.
Kwa mwaka ikiwa ni kati
ya takribani shilingi milioni 240 mpaka milioni 570, kutokana na msamaha wa
madeni ya matibabu kwa majeruhi wa ajali za bodaboda peke yake.
Daktari bingwa wa mifupa
katika hospitali ya Bugando, Dk. Isidor Ngayomela, alisema kuwa wanapokea
majeruhi wa mifupa watatu mpaka wanne kila siku kutokana na ajali za
barabarani.
Kutokana na changamoto
ya gharama za matibabu kuwa kubwa, elimu ya bima ni muhimu kutolewa ili
wananchi wengi wajiunge na mifuko mbalimbali ya bima itakayowasaidia kujilinda
dhidi ya majanga ya ajali kwa kupatiwa matibabu kwa unafuu zaidi.

Comments
Post a Comment